Thursday, November 25, 2010

SIMULIZI YA KUSISIMUA


HADITHI HII TAMU INAENDELEA KATIKA GAZETI LA KIU...HAPA UTAENDELEA KUIPATA KATIKA VIPANDE VIPANDE
MZEE WA SHAMBANa juma kidogo

Pamoja na muonekano wake kuwa ni wa mtu mwenye hali ngumu kimaisha, Bosco Majaliwa au Mzee wa shamba kama alivyojipachika jina, hakuwa mbumbumbu mzungu wa Reli. Pamoja na kutokea kuwa muuwaji wa kutisha, lakini akili yake ilikuwa ikifanya kazi vizuri.


Kuwa muuwaji siyo kipimo cha upunguani, hata wale viongozi madikteta waliopata kutokea miongo kadhaa iliyopita, walikuwa wasomi wazuri wenye akili zao, lakini kwa upande wa pili walikuwa katili na wauaji wa kutisha, watu kama Adorf Hitler, Idd Amin Dada, Irish Ramillienz Sanchez au Carlos na hata Osama Bin Laden ni wauaji ambao wamejiandikia historia isiyofutika kwa kuutingisha ulimwengu.

Hawa pamoja na ukatili wao huo wa kutisha kwa upande wa pili walikuwa na akili zao timamu. Aina hiyo ya binadamu haitofautiani sana na Bosco Majaliwa, tofauti iliyopo ni ndogo sana, “Kipato pamoja na nguvu za uchumi” hiyo ndiyo tofauti pekee inayowatenganisha watu hawa katka umbali wa maili nyingi. Kwa kiasi kikubwa alikuwa amefanikiwa kumuhadaa Inspekta Wabongo kwa kujitenganisha yeye Bosco Majaliwa na Mzee wa shamba kama watu tofauti hali ya kuwa ni yeye huyo huyo mmoja.


Kwa kufanya hivyo alifanikiwa kumficha ‘’mzee wa shamba’’ wa bandia.Alifanikiwa kumuhadaa Inspekta Wabongo, Mzee ambaye alikuwa na uchu na shauku kubwa ya kumnasa muuwaji na kumpa adhabu kubwa na kali ambayo asingeliweza kuisahau mpaka mwisho wa maisha yake, pengine hiyo ingelikuwa adhabu kali ya kwanza kutolewa kwa muuwaji tangu dunia hii ilipoumbwa. Jioni hii Bosco Majaliwa alikuwa amedhamilia kufanya jambo, jambo ambalo lingeendelea kuukwamisha upelelezi wa Inspekta Wabongo, tayari alifanikiwa kumuhadaa na kumpiga chenga ya mwili kwa kuthubutu kufika hadi Ofisini kwake na kuzungumza naye, mara hii aliamua kurudi Ofisini kwa mzee huyo nyakati za jioni wakati giza linakaribisha kushika nafasi na kutawala Anga, nyakati ambazo Inspekta Wabongo huwa tayari keshatoka Ofisini na kwenda zake nyumbani kupumzika ikiwa ni pamoja na kuongea na wajukuu zake. Taratibu aliendelea kusonga mbele kuikaribia Ofisi ya Mzee Wabongo.


Mara hii alikuwa amevalia koti refu jeusi, koti ambalo kwa asilimia kubwa lilifanya afanane na zimwi litembealo usiku, kwa sehemu kubwa koti hilo lilifanya pia afanane na giza. Ofisi za Inspekta huyo zilikuwa ni Ofisi maalumu tofauti na Ofisi za Askari wenzie,hii ilikuwa ni kutokana na umuhimu wake, ni Ofisi ambazo ulinzi wake ulikuwa umeimarishwa na Askari wawili machachari, tena ni wale wa kikosi maalumu cha fanya fujo uone.


Pamoja na Askari hao, pia ukuta wote unaolizunguuka jengo hilo ulikuwa umepambwa kwa nyaya maalumu zilizokuwa zikipitisha umeme wenye nguvu kubwa, umeme huo ndiyo uliwahadaa Askari hao na kupuuza kuzunguuka zunguka jengo hilo na badala yake muda mwingi walikuwa wakiutumia kupiga soga nje ya geti la kuingilia katika Ofisi hiyo, mara moja moja huzunguuka nyakati za usiku wa manane lakini si kwa majira haya ambayo ni mapema kabisa, nyakati ambazo hata kuku bado hawajapata usingizi mabandani mwao.


Ni wakati huo huo ambapo Bosco Majaliwa alifanikiwa kutua ndani ya ua wa jengo hilo, bila wasiwasi wowote aliuendea mlango imara wa kuingilia katika Ofisi za inspekta Wabongo, kwa maarifa yake yaliyochanganyikana na uwezo wake mkubwa wa kufanya mazingaombwe, mlango ule ulisalimu amri na kufunguka bila kipingamizi, sehemu ya kwanza baada ya kuingia katika jengo hilo ilikuwa ni Ofisi ya Stella, Sekretali wa Inspekta Wabongo, hapa kulikuwa na Kompyuta pekee ambayo ilikuwa ikitumika kutunza mafaili na na kumbukumbu zote za ofisi, akaitizama kompyuta hiyo kwa muda wa nukta kadhaa kisha akatabasamu.


Akatabasamu na kutoa mcheko wa kimyakimya, ni mcheko ambao katu huwezi kuisikia sauti yake, akalikunja koti lake vizuri kuelekea kiunoni kisha akakaa katika kiti kilekile akaliacho.Stella kila siku, naye usiku huo akawa mbadala wa Stella, akawasha Kompyuta na kuanza kubofya kitufe hiki na kile, mkononi alikuwa ameshika kitu, ni kitu kilichokuwa kinafanana na nusu ya kidole cha kati cha mtu mzima, kwa lugha ngeni kinaitwa “Frash disk” lakini kwa lugha ya Kiswahili unaweza kukiita “Kidakuzi”.


Baada ya kufanikiwa kupata alichokuwa akikihitaji katika Kompyuta hiyo, akachomeka kile kidude mahali kisha akahamisha mafaili yote yaliyokuwa yamehifadhiwa katika Kompyuta hiyo halafu akainuka na kutoa mcheko ule ule wa kimya kimya, akachomoa kile kidude na kuanza kutoka, lakini alipofika mlangoni akasita kwa muda, kama aliyesahau kitu akageuka na kuanza kuendea mlango wa mbele zaidi, mlango wa Ofisi ya Inspekta Wabongo, kwa mbinu na maarifa yale yale nao akafanikiwa kuufungua na kupenya ndani hadi ilipokuwa meza kubwa ya Mzee huyo, hapo hakuchukuwa muda mwingi, alikusanya kila karatasi iliyokuwa katika meza ya Mzee huyo na kuondoka nazo.


Alipofika nje hali bado ilikuwa shwari kwa upande wake, wale Askari waliendelea kupiga soga huku wakijikumbusha maisha yao yalivyokuwa wakati wakiwa Chuoni. Bosco Majaliwa akaruka ule ua uliokuwa umezunguushiwa nyaya za umeme na kwenda zake.


*** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** ***


Majukumu yalikuwa yamemzidi kimo, mpangano na mlundikano wa majukumu hayo yalifanya aone mchana haotoshi na masaa ya kazi yamepungua mno. Hali hiyo ikamfanya awahi Ofisini mapema zaidi kuliko hata Stella Sekretari wake. Hata hivyo hali ilikuwa tofauti baada ya kufika mlangoni. Mlango ulikuwa umekena ukimcheka na kumshangaa, hilo hakulitegemea, alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa aliufunga mlango kwa funguo makomeo yote pamoja na kuuhakikisha jana yake wakati alipokuwa akitoka ofisini..


Hali hiyo ya kukuta mlango ukiwa wazi ilimuweka katika ombwe na ulimwengu mpya ambao hakuwahi kuufikiria, ulimwengu wa utata mtupu, ulimwengu wa mauzauza, ulimwengu usiofaa kuishi viumbe wa kawaida,yaani ulimwengu wa fadhaa na fedheha.


Kwa dakika nzima alibaki pale pale akiukodolea macho mlango ule asiamini. Mawazo yake yakamtupa kwa wale walinzi maalumu wa Ofisi yake, kwanza akataka kuzihamishia lawama zake kwao, lakini akakumbuka kuwa mlango huo haujavunjwa wala kuchubuka hata kidogo.


Kitu kilichomfanya asite kupeleka lawama moja kwa moja kwa Askari hao ni funguo, funguo zote za Ofisi mtunzaji ni yeye na huondoka nazo kila siku kurudi nyumbani, na hata hapo alikuwa nazo,kwa hiyo kama ushukiwa wa wizi hiyo inamaanisha kuwa mshukiwa wa kwanza alikuwa yeye mwenyewe. Suala la kusahau kufunga mlango huo hakulipa nafasi hata kidogo.


Akapiga hatua kuingia ndani, kitu cha kwanza kukutana nacho ni Kompyuta iliyokuwa imewashwa, akakuna kichwa. Siku iliyopita yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kutoka Ofisini, wakati akitoka Kompyuta hiyo ilikuwa haifanyi kazi, hiyo inamaanisha kuwa Kompyuta hiyo iliwashwa baada ya yeye kutoka Ofisini jana jioni,halafu macho yake makali yakatua ulipo mlango wa kuingilia Ofisini kwake, ulikuwa wazi kabisa kiasi cha kupita hata ng’ombe mzima. Harakaharka akavuta hatua na kuingia ndani.


Katika meza yake ya Ofisi hakukuwa na karatasi hata moja, hapo ndipo alipotambua kuwa alikuwa ameibiwa, tena aliibwa bila milango kuvunjwa. Karatasi na mafaili yote muhimu ya kesi mbali mbali yalikuwa yamepepea na kutoweka. Hasa yaliyokuwa muhimu zaidi ni yale yaliyokuwa yakihusiana na kesi ya mauaji iliyokuwa ikiendelea. Ni dhahiri kwa hatua kubwa aliyokuwa amefikia sasa alikuwa ameporomoka na kurudi kwenye sifuri.Mwizi alikuwa amemkomoa na kumgeuza bwege wa kutupwa.


Inspekta Wabongo akachanganyikiwa vibaya sana na kujikuta akianza kuporomosha matusi mazito ya nguoni. Hadi Stella alipokuwa akiingia Ofisini hapo, alikuta Bosi wake akiendelea kutukana matusi hayo kama mtu aliyepatwa na uchizi, Stella akashika mdomo kwa mshangao lakini Mzee yule hakujali wala kuona aibu, mwisho wa matusi yale akapiga ngumi ukuta kwa nguvu na kusema, “Namtaka akiwa hai au mfu” akakiendea kiti chake kisha akakaa na kuegemea meza, ikawa kama mtu aliyepitiwa na usingizi muda mrefu uliopita.


*** *** *** *** *** *** *** *** *** *** ***

Siku hii ilimkuta Mdoe akiwa na furaha kiasi, furaha ambayo ilitokana na kupokea mgeni. Mgeni ambaye hakumtegemea sana siku hiyo kutokana na kutokuwa na taarifa za ujio wake. Huyu alikuja ghafla sana, mgeni huyo alikuwa ni Mama yake mzazi ambaye alikuwa akiishi mbali na Kijiji hicho. Alikuja kumjulia hali mwanae kwani huko aliko alipata habari za visa, vituko na matukio ya mauaji yaliykuwa yakikikumbuka Kijiji hicho. Taarifa hizo zilimpa mashaka Mama Mdoe, akaamua kufunga safari ili angalau akamuone mwanae apate faraja.


Wakati wakiongea hili na lile pale sebuleni, wakasikia mtu akibisha hodi, sauti ilikuwa ya mwanaume. Mama Mdoe akainuka kwenda kumkaribisha mgeni. Alipofika mlangoni akasita kwenda mbele zaidi, ni dhahiri alishikwa na butwaa. Mtu aliyekutana naye mlangoni hakumtegemea. Mama Mdoe akaanza kurudi ndani kinyumenyume huku akitetemeka mwili mzima. Mdoe alishitushwa sana na hali ile ya ghafla iliyomkumba Mama yake. Kabla hajajua nini cha kufanya, mtu akaingia taratibu pale sebuleni, hakuwa mtu mgeni sana machoni mwake.


Tayari walisha wahi kukutana mara kadhaa, siku ya kwanza kukutana naye ni siku ambayo alikuwa akienda shamba nyakati za jua kali. Mara ya pili mtu huyo alikuja pale pale nyumbani kwake na kuanza kumdai mali. Leo kaja tena, tena kaja wakati mama yake mzazi yupo. Lakini kuna kitu kiligonga ubongo wa Mdoe. Akajiuliza ni kwa nini Mama yake alishituka sana baada ya kumuona mtu yule. Wakati huo Mama yake Mdoe alishakaa kwenye kochi huku mkono wake wa kulia akiwa kashikilia kwenye titi lake la mkono wa kushoto, ni dhahiri mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kasi na presha ilikuwa juu sana, wakati huo Bosco Majaliwa nae alikuwa tayari kesha jikaribisha katika moja ya kochi dogo sebuleni hapo.


Ni wakati ambapo mawazo ya Mama Mdoe yalihama pale na kumpeleka miaka kadhaa nyuma kipindi ambacho mumewe Mzee Sambusa alikuwa hai. Picha zote za matukio yaliyopita zikaanza kumjia taratibu na kuanza kukumbuka siku moja marehemu mumewe alipomletea taarifa kuwa rafiki yake wanayefanyanaye biashara ya mbao nyekundu amefariki dunia kwa ajali ya gari alilokuwa amepakia mbao zake, hivyo yeye Mzee Sambusa akiwa kama mshirika wa kibiashara na rafiki wa karibu wa marehemu huyo, anafuatilia mzigo huo ili aukomboe usipotee bure, kweli baada ya siku mbili Mzee Sambusa akamletea tena taarifa mpya kuwa maiti ya marehemu rafiki yake tayari imekwisha zikwa iliyobaki ni kwa yeye kushughulikia soko la mbao zile. Taarifa za mumewe aliziamini kwani hakumuona tena mtu huyo mpaka alipomtokea ghafla leo hii, je mtu huyu amefufuka kutoka wafu, Mama Mdoe akavuta pumzi ndefu na kuzishusha kwa mkupuo.


Nafasi ambayo Bosco Majaliwa aliitumia kwa kusema “Sikufa, ningekufa nisingekuwepo leo. Saa hizi ningekuwa nimebaki mifupa mitupu chini ya aridhi, lakini sikufa, tangu wakati huo nipo hai. Ila alichonifanyia mumeo ni kitendo kibaya sana, wewe alikudanganya. Alikudanganya kuwa nimekufa kumbe haikuwa hivyo, leo nitakusimulia kwa kifupi ni nini ambacho kilitokea na mtoto wake huyu asikie kwa masikio yake “ akasema huku akimyooshea kidle Mdoe, Bosco Majaliwa akakohoa kidogo kuweka koo lake sawa kisha akaendelea ''kwanza ni lazima mjue kuwa napo kazini,nipo kazini katika kudai haki yangu “Ilikuwa hivi.


Mara hiyo ya mwisho kuachana na mzee Sambusa, yaani marehenu mumeo, nilikuja na mzigo mkubwa sana wenye thamani ya mamilioni ya shilingi. Tena zilikuwa mbao safi nyekundu, katika hizo hakukuwa na mbao hata moja iliyoharibika, achilia mbali kuharibika hata ule uelekeo tu au dalili ya kuharibika haukuwepo. Ni mzigo ambao nilikuwa nimepanga baada ya kufanikiwa kuuza, nijipe likizo kidogo ya kwenda kujipumzisha kwani biashara ile ilikuwa na hekaheka na misukosuko mingi. Kupishana na wanyama wa hatari porini kama Simba, Tembo, Chui na hata Majoka yenye sumu kali ilikuwa ni kitu cha kawaida. Mbali na wanyama wakali hao, pia wapo wale askari wanaolinda mali ya asili, kwa ujumla kazi ile ilikuwa ni kazi pacha na ujangiri, ujangiri ulikuwa Kulwa, ile yangu ilikuwa Dotto. Nakumbuka sana, nakumbuka mpaka leo nilikuwa nimeamua mapumziko yangu ningeenda kutalii na kutulia kwa muda katika Pwani ya Kenya huko mjini Mombasa.


Mtu wa kupumzika na kutulia nae alikuwepo, msichana mrembo aliyekuwa tishio wakati huo, alinipenda sana lakini nilimpoteza baada ya kupata matatizo,haya haya matatizo yaliyosababishwa na mumeo, mumeo ambaye kwa sasa ni marehemu, mumeo ambaye ni baba yake na huyu mwanao Mdoe. Basi kilichotokea baada ya kufika salama na mzigo ule, nikamkabidhi mumeo kama kawaida yetu lakini mambo yakaenda mrama, haikuwa kama nilivuopanga. Akanizidi kete na kunitia ndani kwa kisingizio kuwa mzigo wote umekamatwa na polisi, lakini nilipofanya uchunguzi nikagundua kumbe haikuwa kweli, ule ulikuwa ni mchezo mchafu wa marehemu mumeo.


Mali yangu yote niliyoitafuta kwa tabu, mateso na hatari nyingi ikawa imekwenda na maji” alopofikia hapo pamoja na ujasiri wa kiume aliokuwa nao. Bosco Majaliwa akaanza kububujikwa na machozi mepesi yaliyokuwa yakichirizika kupitia mashavuni mwake. ghafla akatoa ukelele wa ghadhabu huku akipigapiga miguu yake chini kama farasi aliyetekenywa. Ukelele uliofanya Mdoe na mama yake washituke sana na kutaka kukimbia.


Lakini Bosco Majaliwa akatulia tena na kuendelea na hadithi yake hiyo. ‘’Mateso, Mateso, alinifanya vibaya sana mumeo, aliniacha sina hata senti tano, nikawa chizi, uchizi ambao nimepona kwa tabu sana pamoja na kutumia gharama nyingi za ndugu zangu.


Sikilizeni niwaambie, hali ile kweli ilinifanya niwe chizi, mwehu ambaye nilianza kukimbia hovyo mitaani. Ndugu zangu walifanya kazi ya ziada, kazi ya ziada ya kunikimbiza mara kwa mara. Unajua ugumu wa kumfukuza chizi, kazi yake ni ngumu kama chuma cha reli. Kwanza mfukuzaji lazima awe na sifa zifuatazo, sifa ya kwanza lazima awe na mbio,amkimbize chizi kisha ampige ngwala. Sifa ya pili lazima uwe na nguvu, ukishampiga ngwala kamata kisha mtie kabali.


Sifa ya tatu lazima uvae nguo chafu kama yeye kwani chizi huwa na timbwili zito, ukimfukuza chizi huku ukiwa umevaa suti utawashangaza walimwengu. Kumbukeni pia wakati ule wa uchizi wangu nilikula ngwala nyingi sana, hayo ni miongoni mwa mambo yanayonifanya niwe na hasira zaidi kwa wale wote walioshiriki kuihujumu mali yangu. Kiongozi wao ni marehemu baba yako wewe Mdoe na mumeo wewe mama Mdoe


Nimepona, leo nimekuja mbele yako wewe mama Mdoe, shemeji yangu wa zamani. Nimekuja kudai mali yangu ambayo ipo mpaka sasa. Sina ubaya na wewe, wala mwanao Mdoe, mbaya wangu ni mzee Sambusa, angekuwa hai ningemalizana naye. Ningelikuwa najuwa amezikwa wapi, ningelikwenda kufukua kaburi lake kisha nitoe mifupa yake na kuanza kuicharaza viboko, ningeichapa ki kweli kweli mpaka ningeridhika. Sasa basi, maneno yangu ya mwisho ni haya.


Fumbo wafumbie wana, wale wangali wachanga,

Wakishakuwa vijana, huutambua uhanga,

Wakisha refuka sana, hujitolea muhanga,.

Wale wangali wachanga,fumbo wafumbie wana.


Fumbo la mali wafumbie watoto wakiwa bado wachanga, wakisha kuwa vijana huanza kujitambua na kuanza kudai mali yao. Wakisharefuka sana na kuwa watu wazima, huwa tayari kujitolea muhanga ili wamiliki mali yao.Chagueni kati ya mambo haya, mnikabidhi mali yangu kwa maandishi. Jifanyeni kama mnaniuzia mali zote mlizo nazo kwa kisingizio kuwa mnahama kijiji. Kisha wewe Mdoe utaenda kutafuta mali ya jasho lako ambayo utamsaidia mama yako kutatua matatizo madogo madogo, hilo la kwanza. La pili, mkubali kuwa sehemu ya familia yangu, hapo hamjanielewa, inamaana wewe mama Mdoe uwe mke wangu kuanzia sasa ili nami nifaidi, nifaidi kile alichokuwa akifaidi mumeo marehemu mzee Sambusa, hili ni chaguo lenu la pili. La tatu, kama mtakataa yote hayo itabidi niwauwe. Mfe nibaki na mali yangu, nawapa muda wa kufikiri, kesho nitakuja mchana kuchukua jibu langu. Kwa herini”

Bosco Majaliwa akainuka na kuanza kuondoka akiwaacha Mdoe na mama yake wakitizamana. Waliendelea kutizamana kwa dakika tano zaidi huku kimya kikiwa kimeendelea kutawala kila mtu kati yao alikuwa akijaribu kuyatupa mawazo nje ya chumba hicho na kufikiria namna ya kujikwamua katika mtihani ule mgumu, ulikuwa mtihani mgumu kama ule wa kupanda vidato, toka fungu la vidato vya chini kwenda vidato vya juu, walihitaji maandalizi ya kutosha ili kufaulu mtihani huo ilikuwa ni jukumu lao kuchagua kati ya mambo hayo matatu, moja kukabidhai mali yote ikiwa ni pamoja na nyumba, mashamba na mifugo inayofugwa na mama Mdoe, jambo la pili ilikuwa ni ndoa, ndoa ya lazima kaati ya Bosco Majaliwa na mama Mdoe, jambo la mwisho lilikuwa baya zaidi, kifo, kifo ndilo lilikuwa chaguo lao la tatu waliendelea kuwaza na kuwazua bila kupata muafaka, ni dhahiri walikwama.Ghafla Mdoe akaangua kilio,mwanaume akaangua kilio mbele ya mama yake mzazi.


*** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** ***


Ulikuwa ni usiku tayari, kama kawaida yao baadhi ya watu wa mjini hawalali usiku, usiku kucha hurandaranda kwenye kumbi za starehe wakitafuta maeneo mazuri ya kufanya burudani. Asilimia kubwa ya watu hawa ni vijana. Magari madogo madogo yanayobeba abiria mijini maarufu kama taxi nayo yalikuwa yakizunguka huku na kule kuwakusanya watu na kuwapeleka katika maeneo hayo ya kuponda mali kufa kwaja. Usiku huo ulimkuta Stella sekretari wa Inspekta Wabongo naye akiwa na shauku ya kwenda kujirusha katika moja ya kumbi za disco mjini hapa. Tamaa yake ikamfanya ajikute ndani ya ukumbi maarufu mjini Dodoma ujulikanao kwa jina la CLUB 84, Stella hakuwa na umri mkubwa ambao ungefanya iwe kizuizi kwake kuibuka maeneo kama hayo.Miaka 33 aliyokuwa nayo ilimuweka katika kundi la vijana ambao bado walikuwa umbali mkubwa sana kuukamata uzee.


Ndani ya ukumbi kulikuwa na vijana wengi wa kila rika , wanawake kwa wanaume. Kama kawaida mbali ya muziki mzito kulikuwa na mambo mbalimbali yaliyochagiza na kuongeza uzito wa burudani, vinywaji vya aina mbalimbali baridi na vikali vilikuwa sehemu ya mchango wa burudani hiyo.


Kivutio kikubwa kilikuwa ni aina ya mavazi ya warembo, vikaputura vifupi vifupi vilivyokuwa vimeacha sehemu kubwa ya miili yao ikiwa tupu vilikuwa vimetawala na kuleta hamasa kwa baadhi ya wanaume ambao huwa hawapati lepe la usingizi bila kufanya ngono. Stella akajichagulia meza moja iliyokuwa tupu na kutulia huku akinywa bia yake taratibu, hakuwa mpenzi wa kucheza muziki hivyo muda wote macho yake alikuwa kayaelekeza sehemu ya katikati ya ukumbi ambapo kundi la vijana lilikuwa likiruka majoka kwa muziki wa aina tofauti tofauti, wakati hayo yakiendelea ndani ya ukumbi huo, katika mlango wa kuingilia ukumbini hapo kulikuwa n;a mabishano makali yakiendelea kati ya mabaunsa, wale walinzi maalumu wa mlangoni na mtu mmoja ambaye alikuwa akitaka kuingia ukumbini humo bure bila malipo.


Mtu huyo alikuwa kavalia shati jipya la mtumba pamoja na suruali ya jinsi iliyombana, miguuni alivaa viatu vyeupe aina ya raba huku kichwani nywele zake zilizokuwa zimekolea piko dawa maalumu ya kubadilisha nywele na kuzifanya ziwe nyeusi sana zilikuwa zimechanwa vizuri katika mtindo wa panki. Hata hivyo pamoja na jitihada zake za kutaka kuingia ukukmbini humo kwa nguvu, mwishowe ziligonga mwamba. Kwa muda wa dakika kadhaa akabaki akiwa katizamana na mabaunsa wale asijue la kufanya. Akaendelea kuzunguka zunguka maeneo yale hadi usiku wa manane, usiku ambao baadhi ya watu walianza kutoka mmoja mmoja katika ukumbi huo. Stella alikuwa mmoja kati ya watu hao, alipofika mlangoni macho yake yakagongana na macho ya mtu mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake akimtizama yeye kwa umakini mkubwa.


Stella ghafla moyo wake ukashituka na kuongeza kasi ya mapigo yake. Haukuwa mshituko wa uoga, bali ulikuwa ni mshitukko wa kawaida. Pamoja na kuwa mtu yule alikuwa kajibadilisha kwa kiasi kikubwa kwa kuvaa nguo tofauti na alizozoea kuvaa siku zote na nywele zake alizipaka piko ili kuficha mvi zisionekane. Stella alimtambua, alikuwa ni Bosco Majaliwa, mtu yuleyule aliyetokea Kupenda katika mazingira ya kutatanisha. Bosco Majaliwa akaachia tabasamu pana lililoashilia mapenzi, tabasamu ambalo lilifanya nusu ya meno yake kuonekana kinywani, ndipo Stella alipogundua kwa mara ya kwanza kuwa mtu yule alikuwa na mwanya kati ya meno yake ya juu. Mwanya uliomkumbusha mbali sana, ulimkumbusha miaka ya nyuma wakati ambapo alikuwa mgeni wa mapenzi.


Mpenzi wake wa kwanza alikuwa na mwanya kama huo, bila kujitambua Stella nae akajikuta akitabasamu. Bosco Majaliwa akasema “Nimekusubiri wewe hapa kwa muda mrefu, nilikuona tangu ulipokuwa ukiingia ukumbini, kwa kuwa nilijuwa ni lazima utatoka. Nikaamua kukusubiri hapa hapa nje, najua umechoka sana lakini nina mazungumzo na wewe, tunaweza kuongea kando kidogo au kama hutajali, twende tukaongelee ndani ya gari lako, unipe lift pia kwani hata mimi naelekea hukohuko mjini uendako wewe”. Ni kweli Stella alikuwa amechoka sana lakini kutokana na kuizoea ile tabia ya kiaskari, akaona hakuna sababu ya kupuuza kumsikiliza mtu huyo, kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, akaamua aondoke nae.


Wakati wakiondika wale wanaume waliokuwa wakimmezea mate ya uchu Stella wakaachwa na mshangao, walishangaa kutokana na utofauti mkubwa uliokuwepo kati ya Stella na Bosco Majaliwa, Stella alionekana kuwa ni babu kubwa na msichana wa bei mbaya wakati Bosco Majaliwa alionekana kama kapuku tu, mtu ambaye maisha yamempiga chenga ya mwili na kumpitia kushoto. Lakini huo ndio utamaduni wa mapenzi, mapenzi hayana macho, ni kama upofu, popote pale unapita, walipoingia kwenye gari Bosco Majaliwa akaanza kwa kusema “Utanisamehe sana kwa haya nitakayoyasema kama kwa namna moja ama nyingine nitakuwa nimekukera, lakini si matusi. Ni maneno ya kawaida, maneno mazuri ambayo wanawake wengine waambiwapo huchukia na kuanza kutukana matusi ovyo” Stella alikuwa kimya akimsikiliza huku akiendesha gari kwa mwendo wa taratibu sana” Bosco Majaliwa akaendelea huku macho yake akiwa ameyaelekeza mbele.


Wanawake wengine humdharau mtu kutokana na muonekano wake, hilo ni kosa kubwa sana kwa binadamu, mwenyezi Mungu anapomuumba binadamu, hamnyimi kila kitu, anaweza kukupa utajiri wa mali lakini akakunyima utajiri wa mapenzi, anaweza kukupa utajiri wa mapenzi akakunyima ule wa mali, na mambo mengine chungu nzima, haya ninayoyasema yapo na yataendelea kuwepo hadi masiha atakapoichungulia Dunia kutokea mbinguni wakati wake wa kurudi utakapofika, mimi ni masikini, sina mali, huo ndiyo ukweli. Lakini pamoja na umasikini huu, haujafanikiwa kunifanya nisipende.Yatosha tu kusema kwa kifupi kuwa, nakupenda sana Stella” aliposema hivyo mwili wa Stella ukasisimka sana na macho yakaanza kumlegea, hali hiyo ilianza kumpata tangu walipoonana na mtu huyo kwa mara ya mwisho kule Ofisini, akapiga moyo konde kwa kujipa matumaini “Si siku moja tu” akawaza. Alikuwa na nafasi kwani nyumbani kwake alikuwa akiishi peke yake. Safari yao ikawa imeishia hapo. Stella akajikuta ametumbukia katika penzi la muuaji bila ya kutambua.
***************************
Bosco Majialiwa aligeuka na kuwa mtu wa pande mbili, upande mmoja awapo kijijini alikuwa akibadilika na kuwa mtu mwenye hasira, chuki na kisasi. Lakini anapokuwa katika mazingira ya mjini huwa ni mtu mwenye furaha, upendo na hekima pia. Pamoja na kuwa muonekano wake ulikuwa wa mtu duni, lakini uwezo wake wa kufikiri ulikuwa wa kiwango cha juu sana.

Kambi iliyowekwa na askari wale kijijini matumbulu ilikuwa ikimkera kuliko kitu chochote, hakuwa na namna yoyote ya kuwadhibiti askari hao zaidi ya kubuni mpango wa kuiteketeza kabisa kabisa kambi hiyo. Ndipo alipoamua kutengeneza bomu la kienyeji. Lilikuwa ni aina ya bomu linalotokana na nguvu mbili mchanganyiko. Nguvu ya kwanza ilikuwa ni ile ya sayansi ya kawaida, kwa hii alihitaji baruti na petroli. Nguvu ya pili ilikuwa ni ile ya sayansi ya asili, hii ilikuwa kubwa kuliko ile ya kwanza na mara nyingi madhara yake huacha utata na maswali mengi nyuma yake. Aliamua kutengeneza bomu la kuiangamiza kambi ile kwa kuamini kuwa askari wale walikuwa wakimchelewesha sana kufikia malengo yake.


Umasikini ulikuwa umemchosha sana, ilimuuma sana maisha aliyokuwa akiishi. Maisha ambayo yalikuwa yamechagizwa na mpuuzi mmoja , ambaye ni marehemu, mzee Sambusa. Mawazo hayo ndiyo yaliyofanya kasi ya kutengeneza bomu hilo iongezeke. Alipanga kwenda kuilipua kambi hiyo siku hiyohiyo, tena mchana kweupe huku watu wakishuhudia. Huo haukuwa mpango mpya, ulikuwa ni mpango alioanza kuufikiria tangu siku ya kwanza askari wale walipoingia kijijini hapo. Bomu alilokuwa akilitengeneza lilikuwa halina viwango wala kipimo cha madhara yatakayotokea. Mabomu ya aina hiyo huwa hayatabiriki, ni mabomu pata potea. Linaweza kuangamiza kijiji kizima pamoja na mlipuaji, ama linaweza lisiuwe hata nzi.


Lilikuwa ni aina ya bomu la kubahatisha sana. Aina hii ya mabomu hutumiwa sana na wale walipuaji wa kujitolea muhanga, kwa mtumiaji wa kawaida kama Bosco Majaliwa lilihitaji zaidi ya umakini wa kawaida. Pembeni ya kichaka mahali penye manyasi mengi Bosco Majaliwa alikuwa akiendelea kufunga hiki na kile kikiwa ni pamoja na kuchanganya dawa mbalimbali za asili. Kulikuwa na mkusanyiko wa vitu mbalimbali vikiwemo manyoya ya Nyumbu motto, ungaunga wa mifupa ya ndege aina ya Kunguru pamoja na mafuta ya Simba yaliyochanganywa na nyongo ya Mamba, katika vitu vyote hivyo mavi ya Tembo pia yalikuwepo. Mchanganyiko wa vitu vyote hivyo ulikuwa umechanganywa kitaalamu pamoja na baruti ya kawaida. Kulikuwa na kibuyu maalum kilichokuwa kimejazwa lita kadhaa za petroli, tena ilikuwa ni ile petroli supa isiyochakachuliwa. Ni petroli ambayo hulipuka hata mahali palipo na jua kali au joto linalozidi sentigredi 50 tu. Petroli ambayo aliitunza kwa muda mrefu sana kwani alijua siku moja itafika ataitumia kwa kulipiza kisasi.


Bomu lake hilo la kienyeji tayari lilikuwa limekamilika kwa ajili ya matumizi. Kadri lilivyokuwa likikamilika ndivyo hasira zake zilivyokuwa zikizidi kupanda, safari hii alikuwa na shauku na hamu kubwa ya kubangua ubongo wa binadamu kwa mkupuo, alipanga kufanya tukio ambalo litawafanya watu wote wawe na hekaheka hivyo hufanya iwe rahisi kwake yeye kumalizana na Mdoe. Baada ya maandalizi yote kukamilika akachukua bomu lake na kulitumbukiza kwenye mfuko wa plastiki aliokuwa nao, taratibu akaanza kuondoka. Mzigo huo ulitakiwa kubegwa kwa uangalifu mkubwa sana kwani haukutakiwa kutingishwa. Aina hiyo ya bomu ilitakiwa kupigwa mchana tu wakati wa jua kali muda ambao huwa na joto kali, wakati wa baridi kali hasa nyakati za usiku aina hiyo ya bomu huwa halilipuki.


Uamuzi wake ulikuwa wa haraka sana, akaanza kutembea taratibu kurudi kijijini wakati huo ilikuwa tayari mchana umewadia na njia za kijijini hazikuwa na watu wengi kutokana na kuwa wengi wao walikuwa mashambani, wale wachache waliobaki majumbani wengi wao walikuwa ni wanawake na watoto,labda na wale wanaume wavivu ambao hawakuwa na mashamba,katika hao wenye wivu pia walikuwemo kwani waliona tabu kuwaacha wake zao nyumbani kwa hofu ya kuibiwa. Kutoka pale alipokuwa haikuwa umbali mrefu sana hadi kufika maeneo ya katikati ya kijiji. Tokea kuuwawa kwa Koplo Wambura kambi ya askari hao ilkuwa imeimarishwa sana. Mahema yote yalikuwa yamezungushiwa mkanda wa njano uliokuwa na maandishi mengi yaliyokuwa yakisomeka Polisi line danger, Polisi line danger, Bosco Majaliwa akiwa na mfuko wake mkononi aliipuuza amri ile na kuvuka uzio sasa akawa anasonga mbele kuyaendea yale Mahema. Kwa bahati mbaya kwa upande wake askari wale walikuwa wamepewa amri ya kumfyatulia risasi mtu yoyote atakayeingia katika uzio huo bila sababu maalumu.

Wakati Bosco Majaliwa akianza kujiandaa kutupa lile fuko lake yalipo yale Mahema, askari mmoja akamuona, kwa kasi ya ajabu akainua bunduki yake na kumlenga Bosco Majaliwa, sekunde iliyofuata mlio wa risasi ukasikika. Lilikuwa ni tukio ambalo Bosco Majaliwa hakulitarajia asilani, risasi ile ikampata kwenye bega lake la kulia. Tendo lililofanya aurushe mfuko ule na kudondokea mbali kidogo. Wakati askari yule akijaribu kumlenga Bosco Majaliwa kwa mara ya pili fuko lile likawa limetua chini karibu na Hema mojawapo miongoni mwa yale yaliyokuwa yamejengwa katika eneo lile.


Kishindo kikubwa sana kikatokea kikifuatiwa na mlipuko mkubwa, mlipuko uliosikika katika eneo kubwa hadi Dodoma mjini. , kishindo ambacho kilitikisa Vijiji vya jirani pia. Watu Kijijini Matumbulu wakaanza kukimbia huku wakiacha nyumba zao na kutawanyika hovyo. Wale waliokuwa mashambani nao wakatupa majembe yao na kukimbilia makorongoni kwenda kunusuru roho zao, hali ilikuwa ya kutisha na kuongofya sana,


Vumbi kubwa lilitimka likiwa limeambatana na moshi mwingi uliosababisha wingu zito kutokea hewani,wingu ambalo kwa sehemu kubwa lilisababisha miale ya jua isivifikie viumbe hai virukavyo,kutembea na kutambaa juu ya aridhi .hakuna aliyefahamu undani uliosababisha kutokea kwa tukio hilo.isipokuwa wapo waliosema ni nguvu za giza,wengine wakasema inawezekana ile ilikuwa vita kati ya Malaika na Shetani.


Watoto nao walionekana wakitimua mbio kukimbilia Makanisani na Misikitini huku wakipaza sauti hewani kuwa mwisho wa dunia umefika,baadhi yao walisema hilo lilikuwa bomu la Nyukria lililodondoshwa kimakosa na ndege ya kivita ya Korea kaskazini iliyokuwa ikipita juu sana angani.Tukio hilo lilishuhudiwa pia na mtu mmoja aliyekuwa kwa mbali sana.Mtu yule alilichunguza wingu hilo kwa muda na kushindwa kutambua ni aina gani ya mvua ilikuwa ikitaka kunyesha,mvua ya aina yake ambayo katika umri wake wa miaka zaidi ya 60 hakuwahi kuona aina ile ya mawingu.Alizoea kuona aina za mawingu kama Ngamba,Mdaa nk.Lakini hayo yalikuwa mapya sana kwake,japo yalimshangaza,lakini alijilazimsha kupuuza tukio lile na kurudi ofisini.


Alipoingia tu ofisini akakutana na makele ya mvumo wa simu yake ya ofisini,ili kupunguza ghasia na kero hiyo.Akaamua aipokeeharaka haraka,’’hallow’’ upande wa pili ukaita na kusema, ‘’kumetokea tukio la ajabu sana hapa kijijini Matumbulu ambalo huenda likawa limesababisha watu kadhaa kpoteza maisha’’upande wa pili ulisikika ukisema simuni.Akakohoa kidogo kisha akauliza ‘’ni tukio gani hilo?’’ upande wa pili ukaendelea,’’haijulikani kama ni vita,mlipuko wa bomu au kitu gani.Kama ni bomu basi laweza kuwa ni zaidi ya skadi’’ kama siyo bomu basi inawezekana ni mlipuko wa Volkano.Inspekta wabongo akakaa kimya bila kusema chochote mpaka simu ilipokatika yenywe.


Inspekta Wabongo akaanza kutembea tembea Ofisini kwake huku akikuna kichwa, ni dhahiri unga wa ugali ulikuwa umezidi maji, bora maji yangezidi unga lakini hali hiyo ilikuwa ni sawa na unga kuzidi maji, mzigo ulikuwa umeongezeka mara dufu, alikuwa na kazi kubwa. Kazi ambayo ni kama alikuwa ameziliwa na jeshi hilo, Viongozi wote na maafisa wa jeshi hilo katika ngazi za juu walikuwa wamechanganyikiwa kuliko yeye. Kila mtu alikuwa hajui aanzie wapi aishie wapi. Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa nayo ilikuwa imeandaa tume maalumu ambayo ilikuwa imepanga kwenda Kijijini Matumbulu kwa ajili ya kufanya uchunguzi. Uamuzi huo Inspekta Wabongo hakuupenda, alitaka kazi hiyo waachiwe Polisi na siyo watalii, wansiasa huwa anawafananisha na watalii au mabingwa wa uongo. Aliifananisha tume hiyo na watalii kwani aliamini kuwa huko hakuna lolote la maana watakalofanya zaidi ya kuongea na wanakijiji mambo ya utawala.


Wakati huo shida yake yeye ilikuwa ni kumpata muuwaji akiwa hai au amekufa,na wala siyo ibada za ujenzi wa Zahanati au Madarasa. Ndipo alipopata wazo jipya. Kumtumia mpelelezi wake wa siku nyingi ambaye aliachana na jeshi hilo na kutoweka zaidi ya miaka miwili iliyopita. Japo walikuwa wakiwasiliana mara moja moja kwa njia ya mtandao, lakini hakuwahi kumwambia alipo. Ni kama mtu aliyekuwa kajificha mahali asitake kuonekana. Wazo la kumbebesha kazi hiyo Benjamin Rorges au Ben Roja kama walivyozoea kumwita akaona kuwa kwa kiasi Fulani litakuwa limempunguzia mzigo katika ubongo wake. Akaamua afanya naye mawasiliano haraka iwezekanavyo.


*** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** ***


Alikuwa kajipumzisha huku akipitia magazeti mbali mbali ya nchini mwake kupitia mtandao wa simu yake. Habari kubwa iliyokuwa imetawala magazeti mengi kwa siku hiyo ilimsisimua sana, gazeti la kwanza liliandika, tetemeko kubwa laukumba mji wa Dodoma. Gazeti lingine likaandika, Dodoma yakumbwa na dharuba. Lakini alipofungua gazeti jingine lilikuwa limepambwa na kichwa cha habari tofauti kidogo na hayo mengine, hili lilimvutia zaidi. Kichwa cha habari kilichokuwa kimepambwa kwa maandishi makubwa meusi kilisomeka, ‘’Bomu kubwa la nyukria lalipuka nje kidogo ya mji wa Dodoma’’, hata hivyo alipoifuatilia kwa undani habari hiyo akakuta kuwa ilikuzwa sana na kichwa chake cha habari kwani madhara ambayo yangesababishwa na mlipuko huo hayafanani kabisa na madhara ambayo yangesababishwa na Bomu la Nyukria, akajua hizo zilikuwa ni mbwembwe za mhariri za kulinadi gazeti lake ili nakala zake zinunuliwe kwa wingi.


Baada ya kuchoka kusoma magazeti hayo akaona afungue pia anuani yake ya barua pepe ili aone kama kuna ujumbe wowote umeingia. Hiyo ilikuwa ni kawaida yake, kila siku apatapo muda wa kupumzika ilikuwa ni lazima afanye hivyo. Ni kweli alikuta ujumbe, ujumbe uliokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka “UJUMBE MUHIMU” baada ya kusoma ujumbe huo ndipo alipogundua kuwa magazeti yale yalikuwa yakimaanisha nini. Huo ulikuwa ni ujumbe maalumu kutoka kwa Bosi wake wa zamani Inspekta Wabongo.


Kwa kiasi fulani akapata faraja baada ya kutambua kuwa amani imevurugika huko nyumbani, binafsi tangu alipotoweka Tanzania tayari alishazoea kuishi katika mazingira ya kutatanisha. Tangu alipotoweka ghafla zaidi ya miaka miwili iliyopita Ben Roja alianza kazi ya Udereva maalumu wa kusafirisha magari kama Dereva wa kukodiwa kutoka bandari ya Dar - es - Salaam na kuyapeleka huko katika nchi za Magharibi mwa Tanzania, yaani Congo, Rwanda na Burundi. Ilikuwa ni kazi iliyokuwa ikimpatia kipato kizuri hivyo maisha yake yalibadirika na kuwa ya kifahari. Kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo, hakuridhika na kile alichokuwa akikipata, akaendelea na kazi yake hiyo. Lakini ikaja kutokea mkosi katika moja ya safari zake akajikuta akiangukia mikononi mwa majeshi ya waasi ya Jenerali Nkunda yaliyokuwa yamejiimarisha huko mashariki mwa Congo.


Haikuwa rahisi tena kuchomoka katika kundi hilo baada ya Uongozi wa kundi kubaini kuwa Ben Roja alikuwa kaiva katika nyanja ya upambanaji wa kutumia siraha na hata ule wa kavu kavu yaani mikono mitupu, mwanzo alikuwa akipata mateso makubwa sana lakini baadae akawa ni miongoni mwa watu wenye heshima katika kundi hilo. Lakini hata hivyo hakudumu sana katika kundi , akaamua kutoroka. Kitu kikubwa kilichofanya atoroke ni ukatili wa wanajeshi waliokuwa wakilitumikia jeshi hilo. Uuaji na ulaji wa nyama za Nyani pamoja na binadamu wafupi wanaojulikana kama Mbilikimo vilikuwa ni vitu vilivyokuwa vikimkera sana.


Lakini hata hivyo pamoja na juhudi alizofanya kuwapiga chenga wanajeshi hao akajikuta kaangukia kwa wapigania Uhuru wa jimbo la Kusini mwa Sudani lijulikanalo kama Dafur. Jimbo lililokuwa katika mapambano ya kutaka kujitenga na Serikali ya Sudani Kaskazini. Hata hivyo ssafari yake ya kufika huko haikuwa rahisi, ilibidi atumie uwezo wake wa ziada kuvikwepa vikosi vya wapiganaji wa msituni vijulikanavyo kama Lord Resistance Army (L R A) vilivyokuwa vimejichimbia na kutapakaa kwenye misitu minene huko Kaskazini mwa Congo vikiwakwepa Askari wa jeshi la Uganda. Mpaka alipoitwa nyumbani kwa kazi maalumu na Inspekta Wabongo, alikuwa amekodiwa na kupata dili la ukufunzi katika vikosi vya El Shabab huko Somalia akiwa kama mkufunzi mwandamizi daraja la kwanza.


Safari yake ya kurudi nyumbani ilikuwa ya siri sana kwani hakutaka Wasomali hao wajue kwa kuogopa kumnyimwa ruhusa. Hata hivyo alijisikia unyonge sana baada ya kukanyaga ardhi ya nchi yake kutokana na hali ya hewa aliyokutana nayo. Alikuwa amezoea kusikia milipuko ya makombora kila kukicha, milio ya ndege za kivita pamoja na vishindo vya vifaru ilikuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Hali aliyoikuta nyumbani hakuipenda sana na ilimchosha kwa muda mfupi, milio ya Vyura, Panzi, Chiriku na Mifugo ya aina mbali mbali ilikuwa tofauti sana na vishindo vizito alivyozoea kuvisikia kila siku. Kwa ujumla alikerwa sana na hali ya amani aliyoikuta nchini mwake. Asubuhi hii alikuwa nyuma ya meza ya Inspekta Wabongo akipitia baadhi ya vifungu katika ripoti mpya iliyoandiliwa na Mzee huyo baada ya ile ya mwanzo kuibiwa.


Baada ya kuisoma kwa makini akainua kichwa na kumtizama Inspekta Wabongo kwa macho ya udadisi kisha akacheka kwa dharau na kusema. “Kwa hiyo Inspekta umeniita ili nije nikukamatie mchawi au siyo” Inspekta Wabongo akatoa jicho, hakutarajia dharau ile kutoka kwa yule kijana. Kijana aliyekuwa akimuamini sana tangu zamani “Siyo mchawi, sema ni zaidi ya mchawi” Inspekta Wabongo akasema.Ikawa zamu ya Ben Roja kushangaa “Ok” hakuna neno, ripoti nimeiona, niachie muda wa kupumzika leo. Kesho nitajua nianzie wapi? Kwa mara ya kwanza Inspekta Wabongo akatabasamu baada ya kipindi kirefu sana kupita bila kufanya hivyo.Akainua glasi yake ya mvinyo na kugugumia kwa kuunywa wote uliokuwa umebakia,Ben Roja akamtumbulia jicho na kumshangaa sana.Tangu alipoanza kuishi Sudan na Somalia alianza kusahau aina ile ya vinywaji.Huko alikuwa akiishi na waislamu wenye imani kali.


*** *** *** *** *** *** *** *** *** **** *** ***

No comments:

Post a Comment